Tarehe naikumbuka, ni sita wa ishirini
Kamwe haitaondoka, itasalia moyoni
Ulikuwa wa mashaka, usiku wake yakini
Watu wangu wadhikika, kwa kushushiwa balaa
Tangu Konde ya Msuka, na Kangagani Kojani
Nako Tumbe kadhalika, hadi Nungwi na Kinuni
Na Ngwachani walifika, na Garagara Mtoni
Mote humo ‘meumuka, kwa huzuni zilojaa
Kangagani weondoka, watu wengi masikini
Nyumbanikwe alitoka, Asha Haji wa Hasani
Risasi ikamshika, peupeni uwanjani
Wanawe wayayatika, sita alotuwachia
Abdallah wa Hamadi, kwao Tumbe Mbuyuni
Walimtwanga kusudi, risasi nne tumboni
Mbichi ‘kamuhusudi, aruba wa thalathini
Himkumbuka huzidi, machozi kutandawaa
Hamadi wa Shehe Ali, alikuwa pirikani
Kwao Konde sio mbali, kweupe si machakani
Wempiga mara mbili, risasi za kifuani
Kaacha wake wawili, na mayatima walia
Kombo Hamadi Salimu, miakaye thalathini
Ekuwa kaskatimu, nyumbanikwe barazani
Mara ikaja kaumu, huko kwao Kangagani
Wakazimimina njumu, rohoye wakaitwaa
Chudi Salimu Fadhili, yatima huyu yakini
Kinda bichi na mkweli, kumi na sita sinini
Risasi ya asikari, ikampenya mbavuni
Wingwi Mafya yedhihiri, bado ‘mepigwa butwaa
Mjukuu wa Mjaka, Mohamedi Khalfani
Wawi kwake kamfika, majeshi ya Saimoni
Kijana bado awaka, thineni wa ishirini
Risasi kampachika, kama wapigavyo paa
Kijana Omari Juma, Mwembe Makumbi nyumbani
Amekaa kasimama, hana kitu mkononi
Junudi wakalituma, risau lisimkhini
Hadi Siku ya Kiama, itawaka yake taa
Bayusufu wa Shaame, babuye ni Muhidini
Na wenziwe wanaume, walikuwa barazani
Kamvamia mandeme, kwao jimbo la Kojani
Hicho kipigo ‘siseme, akaihama dunia
Kuna Saidi Makame, wa Garagara Mtoni
Miaka kumi na nane, mtoto wa masikini
Alipigwa nyundo nane, na marungu thalathini
Walitaka asipone, na Mungu akamtwaa
Naye Musa Haji Musa, wa Nungwi kasikazini
Miaka kumi na tisa, ndiyo kwanza ashaini
Risasi ikamfisa, Kivunge akenda chini
Nduguze wajipangusa, machozi ‘mewazidia
Ali Saidi wa Kombo, kwetu Wingwi Kinazini
Risasi moja ya shingo, ikamkata kooni
Kama vile Chumu Kombo, yeye kwao Micheweni
Hayatakwisha kitambo, machungu yalotujaa
Abubakari Khamisi, aliwania Pandani
Wakamrushia risasi, mule mwake maguuni
Ikavunjika nafusi, kwa kinyongo cha moyoni
Mwisho Ilahi Mkwasi, kamwita akamtwaa
Kuna kijana Saidi, alikuwa Saateni
Kosale kutaradadi, na wake mkokoteni
Bure wakamuhusudi, kwa risasi ya kichwani
Na kisha kwa zao kyedi, uongo kasingizia
Ameri Bin Ameri, Bwejuu alwatani
Wemtwaa kwa kikiri, kenda naye mafichoni
Huko wakamuadhiri, adhara ziso kifani
Mwisho naye kahajiri, Zenji nzima yalia
Na wengi waloumizwa, kwa mwingi uhayawani
Machafu waliyotenzwa, ya nuni na Firauni
Hakika yanaumiza, yachoma mwetu nyoyoni
Na bado yaendelezwa, kuwahujumu raia
Rabbi Wewe ni Hakimu, ya haki yako mizani
Waujuwa udhalimu, ulotendwa visiwani
Nasi ndio madhulumu, twaja kwako Ya Manani
Pitisha yako hukumu, uonayo inafaa
Bonn
2 Disemba 2020