Mshairikasti The Poetcast

Vitabu Nyoyoni

December 02, 2020 Mohammed AlGhassani
Mshairikasti The Poetcast
Vitabu Nyoyoni
Show Notes

Tuna vitabu moyoni, mengi tuliyoandika
Mengi siri za sirini, funiko 'mezifunika
Na japo mwetu ndimini, hatuwezi yatamka
Hata mwetu akilini, hatutaki yakumbuka
Lakini kuyaepuka, hilo haliwezekani!

Humu mwetu vifuani, kurasa zajiandika
Nyingi zisizo kifani, hakuna zinachoruka
Zayaweka hifadhini, siku, saa na dakika
Kuna siku ya Manani, kurasa zitafunuka
Zifike kwa kukufika, mambo yawe hadharani!

Tuna hati ulimini, herufi zilopangika
Qafu na Lamu na Nuni, na Hamza kadhalika
Tuna Swadi, tuna Shini, na shadda ya kupachika
Na irabu za sukuni, twajuwa pa kuziweka
Kwa leo twayavumbika, tumejilisha Yamini!

Winoni humu winoni, muna maneno yafoka
Yanataja kwa mizani, kila kitu kilotuka
Hata kiduchu yakini, wino kinakikumbuka
Kitawekwa andikoni, thumma hakitakauka
Ipite myaka na kaka, sikuye iko njiani!

Twenenda nazo kichwani, simulizi za hakika
Hakika si ya kubuni, mambo yaliyotufika
Kuvamiwa viamboni, na mitwana mijikaka
Watumwa wa Firauni, kwa maguvu kutushika
Leo hatutatamka, lakini pindi mwakani!

Bonn 
05 Novemba 2020