Tutandikeni matanga, tukusanyane wafiwa
Tuwalilie wahanga, roho changa zilotwawa
Walokatwa kwa mapanga, na risasi za vifuwa
Wa Nungwi na Kangangani, wa Tumbe na Madaniwa
Walofatwa majumbani, vichwa vikafumuliwa
Walotupwa majiani, hali washanyofolewa
Tulilie mashahidi, ndugu walodhulumiwa
Dhuluma iloshitadi, ilovitanda visiwa
Itendwayo makusudi, lengo la kutukomowa
Tukaye tuomboleze, makiwa haya makiwa
Machozi tumiminize, kwa waliokashifiwa
Tuliye tusinyamaze, tuliye kwa kutambuwa -
Kwa kutambuwa ambacho, chatugeuza wafiwa
Wapendwa kitupokacho, na mwetu kunajisiwa -
Ni hichi tuaminicho, cha uhuru wa visiwa
Kwa kutambuwa hatuna, wa kutuhani wakiwa
Si Wazungu, si Wachina, wala si Bara Asia
Basi atosha Rabbana, Atosha kutegemewa
Bonn
30 Oktoba 2020